Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (as) - ABNA - Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema ndani ya Qur'an Tukufu anasema:
(اتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ وَأَقِمِ الصَّلَاةَ ۖ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ ۗ وَلَذِكْرُ اللَّهِ أَكْبَرُ ۗ وَاللَّهُ يَعْلَمُ مَا تَصْنَعُونَ).
"Soma uliyo funuliwa katika Kitabu, na ushike Sala. Hakika Sala inazuilia mambo machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Mwenyezi Mungu ndilo jambo kubwa kabisa. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yatenda".
Swali la Msingi ni hili: Ni vipi Sala hukataza maovu?.
Jawabu lipo mwisho kabisa wa Aya hiyo hapo juu.
Kitendo cha sisi kusali mara Tano kwa Siku, Asubuhi, Mchana na Usiku, tunakuwa tunaikumbusha hii nafsi kuwa: Sala hii tunasali kwa kufahamu kuwa Allah (s.w.t) anatuona kwa hili tulifanyalo, kwa maana kwamba: Allah (s.w.t) anatuona tunavyosali.
Sasa basi, Ewe nafsi fahamu ya kuwa wakati huo wa Asubuhi, Mchana na Usiku unaposali tambua kuwa Mwenyezi Mungu anakuona unavyosali, kwa Mantiki hiyo, hata yale matendo mengine ambayo unayafanya Asubuhi, Mchana na Usiku Mwenyezi Mungu pia anayaona.
Hivyo, ikiwa kuna muda unahisi kuwa katika muda huu Mwenyezi Mungu hakuoni au hatakuona, basi utafute muda huo usiokuwa wa Asubuhi, wala Mchana na Usiku.
Ukumbusho huu kwa nafsi, unaifanya Nafsi inapotaka kuyaendea maasi na maovu, basi Sala ile ya wakati ule aliyoisali inamuambia kuwa ni muda tu umetoka kusali!
Mwenyezi Mungu uliyemuamini aliyekuona kwenye Sala, Ndiye anayekuona pia hapa katika hili ovu unalotaka kulitenda, hapo hapo haraka haraka Nafsi inasita na kurudi nyuma na kuacha kuthubutu kufanya ovu hilo.
"Na Mwenyezi Mungu Anayajua mnayo yatenda".
Imeandaliwa na: Madrasat Moa Tanga, Tanzania.
Your Comment